Mgogoro wa Mali wazidi kutandaa Afrika Magharibi: Djinnit

25 Januari 2013

Mgogoro unaoendelea nchini Mali unazidi kutandaa na madhara yake kughubika eneo la Afrika Magharibi na Ukanda wa Sahel.

Hiyo ni kauli ya leo Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Afrika Magharibi, UNOWA, Said Djinnit wakati akilipatia Baraza la Usalama hali halisi ya mgogoro huo ambapo amesema hali ilivyo inadhihirisha utete wa eneo hilo.

Bwana Djinnit ameonya kuwa kadri mambo yanavyoibuka nchini Mali, hatari ya kusambaa na kuondoa utulivu kwa nchi zingine iko dhahiri na hilo limedhihirishwa na jitihada za nchi jirani za kuimarisha ulinzi kwenye mipaka yao.

Amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa makini juu ya uwezo mdogo wa nchi jirani na Mali za kukabiliana na vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa na waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Mali na waasi wa Tuareg yalianza mwezi Januari mwaka jana baada ya waislamu wenye msimamo mkali kuteka baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter