Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UM lateua wajumbe wapya 18 wa Baraza la haki za binadamu

Baraza Kuu la UM lateua wajumbe wapya 18 wa Baraza la haki za binadamu

Nchi 18 zimechaguliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kuanzia leo baada ya uchaguzi uliofanywa na Baraza Kuu la Umoja huo na ambapo utekelezaji wa majukumu utaanza rasmi tarehe Mosi Januari mwakani .

Baraza hilo lenye wajumbe 47 liliundwa mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha uendelezaji na ulinzi wa haki za binadamu duniani kote na uchaguzi huo umefanyika baada ya nchi 18 kumaliza muda wao.

Marekani imechaguliwa kuendelea kwa kipindi kingine kwenye Baraza hilo ambapo mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice amesema Marekani iliamua mawka 2009 kuwa mjumbe ili iwe mstari wa mbele kuendeleza haki za binadamu.

(SAUTI YA SUSAN RICE)

"Marekani inashukuru kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine cha miaka mitatu katika baraza la haki za binadamu. Miaka minne iliyopita tulichukua uamuzi huu kwa kuamini kuwa tunaweza kuboresha kazi za baraza hili kwa kuwemo ndani na si kwa kuwa mtazamaji. Na leo Jumuiya ya kimataifa imethibitisha kukubaliana na uamuzi huo.

Nchi zingine zilizochaguliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Haki za binadamu ni Argentina, Brazil, Cote d’Ivoire, Estonia, Ethiopia, Gabon, Germany, Ireland na Japan.

Nyingine ni Kazakhstan, Kenya, Montenegro, Pakistan, Jamhuri ya Korea, Sierra Leone, Umoja wa Falme za kiarabu na Venezuela.

Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa hukutana Geneva, Uswisi ambapo hujadili hali ya haki za binadamu duniani na kutoa mapendekezo.