Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maliasili zitumike kuleta amani na si migogoro: Ban

Maliasili zitumike kuleta amani na si migogoro: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ametaka hatua zaidi zichukuliwe kuepusha migogoro katika nchi inayochochewa na kuwepo kwa maliasili na badala yake utajiri huo utumike vyema kujenga amani.

Bwana Ban amesema hayo leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kuepusha mizozo itokanayo na matumizi mabaya ya maliasili ambapo ameongeza kuwa laana ya kumiliki maliasili haipaswi kuachwa iendelee kuwa kikwazo cha usalama na maendeleo endelevu ya nchi husika.

Amesema tangu mwaka 1990, takribani mizozo 18 imechochewa na matumizi mabaya ya maliasili kama vile mbao, madini, mafuta na gesi na hadi leo vikosi Sita vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vimepewa mamlaka ya kusaidia nchi mbali mbali kuwa na uwezo wa kumiliki maliasili zilizo chini ya vikundi vya waasi.

Bwana Ban ametolea mfano Afghanistan ambako amesema kumeibuka wasiwasi kuwa pengina ugunduzi wa akiba ya madini yenye thamani ya matrilioni ya dola kunaweza kuibua mzozo mkubwa wakati huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo utajiri wa madini ambao ungeboresha maisha ya wananchi, umetumika kufadhili waasi na kuendeleza ghasia

Katibu Mkuu huyo amesema hakuna nchi yeyote yenye migogoro iliyoweza kutimiza hata lengo moja la milenia na kwamba nchi zinapaswa kutambua kuwa amani ya kudumu na maendeleo baada ya vita vinategemea uhifadhi mzuri wa mazingira na matumizi na usimamizi bora wa maliasili.