Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM uendeleze azma yake ya kuleta amani, maendeleo na usalama: Ban

UM uendeleze azma yake ya kuleta amani, maendeleo na usalama: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema wakati taasisi za kimataifa zinakumbwa na majaribu kutokana na migogoro, ukosefu wa usawa na kutokuvumiliana duniani, Umoja wa Mataifa unalazimika kuendeleza kasi yake ya kuleta amani, maendeleo, kusimamia utawala wa kisheria na kuwajengea uwezo wanawake na vijana duniani kote.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya Umoja wa Mataifa hii leo ambapo amesema jukumu hilo la Umoja wa Mataifa linawezekana kufanikiwa na kupata suluhisho la kudumu iwapo kutakuwepo na ushirikiano kwani hakuna mtu mmoja au nchi moja pekee inayoweza kumaliza changamoto zilizopo.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Hata hivyo tunaweza kufanikiwa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, watendaji wakuu, wanasayansi, wasomi, watoa misaada na viongozi wa kijamii. Hakuna kiongozi mmoja pekee, nchi au taasisi anaweza kufanya vitu vyote. Lakini kila mmoja wetu anaweza kufanya kitu Fulani. Pamoja kama washirika tunaweza kukabiliana na vitisho, tukashinda vita na kutokomeza umaskini.

Katika salamu hizo pia Bwana Ban anakumbusha majukumu ya Umoja wa Mataifa katika sehemu mbali mbali duniani .

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Umoja wa mataifa siyo sehemu ya mikutano ya wanadiplomasia. Umoja wa mataifa ni mlinzi wa amani, hupokonya silaha vikundi vya kijeshi, ni mhudumu wa afya kwani husambaza dawa, hutoa huduma za kibinadamu kwa kusaidia wakimbizi, pia ni mtaalamu wa haki za binadamu kwa kusaidia haki itendeke.

Kuhusu malengo ya milenia, Bwana Ban amesema kumekuwepo na maendeleo ya kutia moyo, umaskini wa kupindukia umepungua kwa asilimia 50 tangu mwaka 2000 na kuna dalili za ukuaji wa kiuchumi na hivyo ni muhimu kuandaa ajenda ya mambo ya kutekeleza baada ya mwaka 2015 ambao ni ukomo wa kipimo cha malengo hayo.