Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wapendekeza mfuko wa kimataifa kwa ulinzi wa kijamii

Wataalam wa UM wapendekeza mfuko wa kimataifa kwa ulinzi wa kijamii

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wamesema ikiwa asilimia 2 ya mapato ya ulimwengu mzima yangetumiwa kwa kuwapa watu maskini ulinzi wa kijamii, watu wote duniani wangeweza kufurahia haki hii ya msingi ya binadam.

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kuwa na chakula, Olivier De Schutter, na yule anayehusika na umaskini wa kupindukia na haki za binadam, Magdalena Sepulveda, wamesema takriban asilimia 80 ya watu maskini duniani hawana ulinzi wa kijamii unaoweza kuwapa kinga kutokana na ukosefu wa ajira, ugonjwa au ulemavu, pamoja na majanga ya njaa na mfumko wa bei ya chakula.

Bwana De Schutter amesema kufuatia ukame ulokuwepo msimu wa kiangazi au Summer Marekani, bei ya chakula ipo juu kwa viwango vya hatari kwa mara ya tatu katika miaka mitano, na njaa imebaki kuwa juu kwa viwango visivyokubalika, kama takwimu za shirika la chakula na kilimo, zinavyoonyesha.