Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zisaidie mashirika ya posta kuwa injini za uchumi wa nchi: UPU

Serikali zisaidie mashirika ya posta kuwa injini za uchumi wa nchi: UPU

Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Mashirika ya posta duniani, UPU, Edouard Dayan amesema huduma za posta hazijadorora katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi na intaneti, bali zinajiendeleza na kutekeleza majukumu yake.

Katika salamu zake hii leo ambapo ni siku ya posta duniani huku wadau wakikutana huko Doha, Qatar kwenye kongamano la 25 la UPU, Dayan amesema huduma za posta ni sehemu ya ulimwengu wa sasa wa digitali na ameyataka mashirika ya posta kubuni, kuendeleza na kuimarisha huduma za posta zitakazotumiwa na watu wote.

Hata hivyo Mkuu huyo wa UPU yenye nchi wanachama 192 amezitaka serikali kutoa usaidizi wa kutosha kwa sekta ya posta ili iweze kuwa injini ya uchumi wa Taifa.