Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi kubwa ya watu bado wanakabiliwa na tatizo la njaa Sahel:UM

Idadi kubwa ya watu bado wanakabiliwa na tatizo la njaa Sahel:UM

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu katika eneo hilo, David Greesly amesema idadi kubwa ya watu katika eneo la Sahel bado wanakabiliwa na tatizo la njaa, Lakini amesema huenda likapungua mnamo mwezi Oktoba, wakati wa mavuno ya kwanza ambapo pia bei ya chakula inatarajiwa kupungua.

Amesema idadi ya watu wanaolazimika kuhama makwao kaskazini mwa Mali imepungua, ingawa zaidi ya watu 451, 000 bado wametoroka makwao kwa sababu ya migogoro. Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa mvua nzuri inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa nafaka kutoka asilimia 5 hadi 17, ikilinganishwa na mwaka ulopita.

Amesema eneo la Sahel linakumbwa na matatizo mengine, kama vile mafuriko, ambayo yanasababisha kusambaa ugonjwa wa kipindupindu, na pia kuna hatari ya uvamizi wa nzige nchini Niger. Ameongeza kuwa wafadhili wameitikiwa vyema ombi la ufadhili kufikia sasa, na hadi asilimia 56 ya dola bilioni 1.6 zilizoombwa zimepatikana.

(SAUTI YA DAVID GREESLY)

Umoja wa Mataifa na wadau wengine sasa wanaangazia jinsi ya kuongeza uwezo wa watu katika eneo hilo kukabiliana na ukame.