Uchaguzi wa rais wa Somalia unafungua ukurasa mpya

17 Septemba 2012

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amepongeza kuchukua madaraka kwa rais mpya wa taifa hili Hassan Sheikh Mohamud akisema kuwa sasa enzi mpya imezaliwa katika taifa ambalo lilisongwa songwa na matukio ya vita na umwagaji wa damu.

Kuchaguliwa kwa rais huyo mpya kumehitimisha kipindi cha zaidi ya miaka nane kilichoshuhudia taifa hilo liliandamwa na machafuko ya kisiasa ambayo pia yamezorotesha ustawi wa watu wake.

Lakini Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo hilo Augustine Mahiga pamoja na kupongeza kwa hatua hiyo, lakini ameitolea mwito jumuiya ya kimataifa kutolitupa mkono taifa hilo ambalo amesema kuwa sasa linaanzisha enzi mpya yenye kuangaza mwangwa uletao matumaini.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuziunga mkono juhudi zinazoanza kuchukuliwa na rais Mohamud ambaye anakabiliwa na changamoto ya ujenzi upya wa taifa hilo ikiwemo pia kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.