Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awapongeza Wasomali kwa bunge jipya

Ban awapongeza Wasomali kwa bunge jipya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amekaribisha kuzinduliwa kwa bunge jipya la taifa nchini Somalia siku ya Jumatatu, kulikofanyika katika mji mkuu Mogadishu. Katika taarifa ilotolewa na msemaji wake, Bwana Ban ametuma risala ya pongezi kwa watu wa Somalia kwa wakati huu wa kihistoria, katika safari yao kwenye barabara ya amani, utulivu na maendeleo ya kisiasa.

Amepongeza ujasiri na kujitolea kwa Kamati ya Kitaaluma ya Uteuzi, na wazee wa kitamaduni nchini Somalia, ambao wamefanya kazi kwa ari, hata wakati wakikabiliwa na mashinikizo mengi, na kuweza kuteua na kuidhinisha bunge jipya ambalo ni lenye kuaminiwa, na kuwakilisha picha kamili ya taifa la Somalia.

Wakati huohuo, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia, Balozi Augustine Mahiga, amekaribisha pia kuapishwa kwa bunge jipya Somalia kama tukio la kihistoria, na kusema Somalia inaanza katika misingi mipya ya uongozi wa kikatiba na kidemokrasia.

Raia wengi wa Somalia wamesambaa kote duniani kwa sababu ya hali ambayo imekuwa nchini mwao kwa zaidi ya miongo miwili. Je, wanaionaje hatua ya kumalizika kipindi cha mpito na kuapishwa bunge jipya? Abdi-Rashid Hussein, ambaye anaishi Kenya, ni mmoja wao.

(SAUTI YA ABDI-RASHID)