Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Asikitishwa na Kushindwa kwa Baraza la Usalama Kuafikia Azimio kuhusu Syria

Ban Asikitishwa na Kushindwa kwa Baraza la Usalama Kuafikia Azimio kuhusu Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameelezea kusikitishwa kwake na kushindwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuafikia azimio la kukabiliana na hali inayoendelea kuzorota kwa kasi nchini Syria.

Amesema matokeo ya kura iliyopigwa leo yanakera, hasa wakati ambapo ari zaidi na shinikizo zaidi lilihitajika ili kuyafikia malengo yaloidhinishwa na Baraza la Usalama, ya kusitisha kabisa ghasia, kuwalinda raia na kuwezesha mpango wa kisiasa wa mpito, ambao ungeleta mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia.

Amesema wakati ni wa dharura, na kwamba jamii ya kimataifa ina wajibu wa pamoja kwa watu wa Syria. Amesema ni dhahiri kuwa serikali ya Syria imeshindwa kuwalinda watu wake. Ameongeza kuwa yeye, mwakilishi maalum wa pamoja, Kofi Annan, pamoja na Umoja wa Mataifa kwa jumla, hawatapoteza juhudi zozote katika kutafuta njia ya kukomesha ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu, na kuweka mfumo wa amani na kidemokrasia wa mpito wenye kutimiza matakwa ya watu wa Syria.

Amesema ni jukumu la mataifa wanachama na serikali ya Syria kukomesha mauaji na matumizi ya silaha nzito nzito katika maeneo ya watu wengi. Amerejelea wito wake kwa pande zote katika mzozo wa Syria kukomesha aina zote za ghasia.