UN yafurahishwa na mazungumzo ya Korea

9 Januari 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha maendeleo yaliyofikiwa kwenye mazungumzo kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kile ambacho kimemvutia zaidi Bwana Guterres ni makubaliano ya pande mbili hizo kushirikiana ili kupunguza mvutano wa kijeshi, kuwa na mazungumzo ya kijeshi na pia kufungua njia nyeti ya mawasiliano kati yao.

Amesema kuanzishwa tena na kuimarishwa kwa aina hizo za mawasiliano ni muhimu sana katika kupunguza hatari ya kutokuelewana na pia kupunguza mvutano kwenye ukanda wao.

Katibu Mkuu amekaribisha pia uamuzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK wa kupeleka ujumbe wake kwenye michezo ya majira ya baridi huko Korea Kusini.

Bwana Dujarric amesema ni Imani ya Katibu Mkuu kuwa kupitia michezo hiyo, Korea Kaskazini ijulikanayo pia kama DPRK, inaweza kuimarisha mazingira ya amani, stahmala na maelewano na mataifa mengine ikiwemo yale ya rasi ya Korea na kwingineko.

Halikadhalika Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kutambua jitihada zilizofanikisha kupunguza mvutano akisema ni matumaini yake kuwa jitihada za aina hiyo zitaendelea ili kurejesha mazungumzo ya dhati yatakayosaidia kuwa na amani ya kudumu na rasi ya Korea isiyo na nyuklia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter