Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay ataka Kuheshimiwa kwa Sheria kwenye Kesi kuhusu Mauaji ya Mwanaharakati nchini DRC

Pillay ataka Kuheshimiwa kwa Sheria kwenye Kesi kuhusu Mauaji ya Mwanaharakati nchini DRC

Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Navi Pillay ametaka kukatwa rufaa kwa kesi inayohusu mauaji ya mwanaharakati wa haki za binadamu raia wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo Floribert Chebeya Bahizire na kutoweka kwa dereva wake Fidèle Bazana Edadi.

Bwana Chebeya alipatikana akiwa ameuawa tarehe mbili mwezi Juni mwaka 2010 viungani mwa mji wa Kinshasa ambapo mahakama moja ya kijeshi iliwahukumu polisi watano kwa mauaji, kukamata kinyume na sheria na utekaji nyara. Kutokana na mauaji hayo mkuu wa Idara polisi nchini DRC alifutwa kazi lakini hata hivyo hakufunguliwa mashataka. Rupert Colville ni msemaji wa Kamishna Navi Pillay.

“Kamishna Mkuu anatoa wito viwango wastani vya kimataifa vitimizwe katika kesi hiyo ya rufaa. Bwana Shebeya alikuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za binadam katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na mauaji yake yalikuwa ya kusikitisha sana kwa wanaharakati wa haki za binadamu katika DRC. Mojawepo ya masuala muhimu hasa ni kwamba, ateuliwe jaji mwenye daraja ya juu ya kutosha, kwani swala hili huenda likawahusu maafisa wa ngazi ya juu zaidi wa polisi, na hilo linatoa hofu.”

Pillay pia amelitaka bingu jipya nchini DRC kubuni sheria za kulinda wanaharakati wa haki za binadamu na pia kubuniwa kwa tume huru ya haki za binadamu. Amesema kuwa ofisi ya haki za binadamu imejitolea kutoa msaada kwa utawala wa Congo.