Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yayataka Makundi Hasimu kuwajibika kuulinda Usalama wa raia Afghanistan

UNAMA yayataka Makundi Hasimu kuwajibika kuulinda Usalama wa raia Afghanistan

Wiki iliyopita, raia 214 wa Afghanistan waliuawa au kujeruhiwa katika matukio 48 tofauti. Mashambulizi ya makundi yanayoipinga serikali yalisababisha asilimia 98 ya vifo vya raia. Matukio mawili ya mashambulizi ya kujitoa mhanga yalisababisha vifo vya raia 38 wa Afghanistan, huku 38 wengine wakijeruhiwa vibaya kwenye mji wa Khost na kwenye hoteli moja kwenye Ziwa Qargha.

Makundi yanayoipinga serikali yamekuwa yakitumia mbinu hizi katika maeneo ya hadhara wanakokwenda zaidi raia wa kawaida. Pia makundi haya yamewalenga raia moja kwa moja, na kusababisha vifo vingi na majeraha makubwa, na vitendo hivi vyote ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hapo jana kuwa makundi yote hasimu katika migogoro ni lazima yahakikishe yanaheshimu sheria za kimataifa za kibinadam na haki za binadamu.

Hapo kesho, Baraza la Usalama litajadili suala la Afghanistan, na ujumbe wa Umoja wa Mataifa Afghanistan, UNAMA unasema, ni wakati wa makundi yanayoipinga serikali kuwalinda raia, na kuhakikisha kuwa mashambulizi yao hayawalengi raia.