Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia zinazoendelea Syria hazikubaliki:Annan

Ghasia zinazoendelea Syria hazikubaliki:Annan

Hali nchini Syria inaweza kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe endapo juhudi zaidi hazitofanyika kumaliza machafuko.

Onyo hilo limetolewa na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu kwa ajili ya Syria Kofi Annan alipotoa taarifa yake kwenye baraza la usalama kwa njia ya video leo Jumanne.

Annan amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba wakati shughuli za kijeshi zimepungua nchini Syria , kiwango cha ghasia na ukatili havikubaliki.

Bwana Annan amesema mpango wa uangalizi wa Umoja wa Mataifa Syria UNSMIS inawezekana ikawa ndio fursa pekee iliyosalia kurejesha nchi hiyo katika utulivu.

(SAUTI YA ANNAN)

“Nina uhakika siwaambii siri yoyote wakati ninaposema kuna hofu kwamba taifa hilo huenda likaingia kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe na athari zake zinatisha. Hatutoruhusu hilo kutokea.”

Usitishaji mapigano ambao ni sehemu ya mambo sita katika mpango wa Annan wa amani ya Syria ulianza kutekelezwa April 12.