Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Migiro ataka azimio la kutambua haki za watu wa asili litekelezwe kwa vitendo

Migiro ataka azimio la kutambua haki za watu wa asili litekelezwe kwa vitendo

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro amesema kuwa wakati kunatimia miaka mitano tangu kuasisiwa kwa azimio linalotambua haki za watu wa asili, zingatio kuu linalosalia sasa ni kupima kwa kiasi gani shabaha ya tamko hilo linafikia malengo yake.

Migiro amesema lazima dunia itambue umuhimu wa kutekelezwa yale yaliyomo kwenye tamko hilo ambalo amesisitiza kuwa licha ya kuwepo kwake, lakini bado jamii ya watu wa asili wanaandamwa na matatizo.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la kimataifa linalojadilia masuala yanayowahusu watu wa asili, Naibu Katibu huyo amehimiza haja ya kuwa na mashirikiano ya pamoja ili kutafutia jawabu ya kudumu ya matatizo yanayowakabili watu  hao wa asili.

Kongamano hilo limewaleta pamoja jumla ya wajumbe 2,000 wanaotoka sehemu mbalimbali na wanatazamiwa kuwa na majadiliano kwa muda wa wiki mbili.