Kuyumba kwa bei za chakula bado ni tatizo kubwa:Sundaram

11 Aprili 2012

Miongo miwili baya ya kuanguka kwa bei za chakula na kupungua kwa uwekezaji katika uzalishaji wa chakula, matatizo katika mfumo wa dunia ya chakula yako bayana tangu mwaka 2006 hali ambayo imeongeza hofu kuhusu kutokuwepo chakula cha kutosha kulingana na mahitaji ya dunia.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wake uliowasilishwa na katibu mkuu msaidizi wa masuala ya uchumi na maendeleo Jomo Kwame Sundaram katika mjadala wa Baraza Kuu kuhusu bei za vyakula na matatizo ya bidhaa .

Amesema hofu kama hiyo inachangiwa pia na mabadiliko ya hali ya hewa kwani hali ya hewa isiyotabirika imefanya uzalishaji wa chakula na bei za chakula kuyumba. Nchi ambazo ni wasafirishaji wakubwa wa chakula nje zimepunguza safirishaji kwa kiwango kikubwa na kusababisha bei kupanda zaidi. Matatizo hayo ya bei za chakula yamewaathiri wakulima wadogowadogo ambao wanalazima kuwa katika hatari isiyokubalika.

Bwana Sundaram katika mjadala huo amesema chakula ni haki ya msingi ya kila mtu na kukosa chakula ni hali isiyokubalika. Ameongeza kuwa usalama wa chakula na lishe ni msingi wa maisha ya binadamu hivyo hatua za kudhibiti kuyumba kwa bei za chakula ni muhimu sana.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter