Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka vizingiti vinavyomkwaza mwanamke kiuchumi viondolewe

Ban ataka vizingiti vinavyomkwaza mwanamke kiuchumi viondolewe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa kuondolewa vizuizi na vikwazo vinavyowaandama wanawake duniani kutojitokeza kwenye masuala ya ukuzaji uchumi.

Ametaja maeneo yanakwamisha wanawake wengi kutoshiriki kikamilifu kwenye masuala ya uchumi kuwa ni pamoja kukosa fursa za kuajiriwa, masoko, upatiaji mikopo pamoja na kukosa fursa ya kumiliki mali.

Amesema mazingira kama hayo yanawarudisha nyuma wanawake na hivyo kuwafanya waendelee kusalia nyuma pale panapohusika na masuala ya uchumi na maendeleo.

Amefafanua kuwa kunaposemwa ni muhimu kwa wanawake kushirikishwa kwenye masuala ya uchumi, kuna maanisha kwamba lazima vizingiti na vikwazo vyote viwekwe pembeni na kuanzishwa mifumo ambayo inaweka uwiano wa moja kwa moja kuhusiana na makundi ya wanawake.