Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wazindua kampeni mpya: ‘Watoto sio wanajeshi’

Umoja wa Mataifa wazindua kampeni mpya: ‘Watoto sio wanajeshi’

Kampeni mpya ya kupinga usajili wa watoto katika vita vya silaha imezinduliwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Kampeni hiyo iitwayo, ‘Watoto sio Wanajeshi’ inaongozwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Watoto katika vita vya silaha, Leila Zerrougui na Shirika la Kuhudumia Watoto katika Umoja wa Mataifa, UNICEF. Ujumbe wa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon umesomwa na Mwakilishi wake,  Bi Leila Zerrougui

(SAUTI YA ZERROUGUI akisoma ujumbe wa Ban)

“Watoto wote wanatakiwa kulindwa, na sio kunyanyaswa. Wanatakiwa wawe shuleni, sio katika majeshi na makundi yanayopigana. Watoto wanatakiwa wajihami ni kalamu na vitabu, na sio bunduki. Kampeni hii inaenda sambamba na juhudi nyingine za Umoja wa Mataifa kama vile mkakati wa Kimataifa wa Elimu Kwanza, ili kulinda haki za watoto na kuwapa utu na fursa za maisha bora.”

Bwana Ban ametoa wito kwa serikali, mashirika ya kikanda na yale yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kutimiza lengo la kutokomeza utumiaji wa watoto na vikosi vyovyote vya serikali ifikapo mwaka 2016.

Akizungumza katika nafasi yake kama Mwakilishi wa Katibu Mkuu kuhusu watoto katikavita vya silaha, Bi Zerrougui amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa serikali zinachukuwa wajibu wa kuendeleza kampeni hii, huku mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yakihusishwa mashinani.

 (SAUTI YA ZERROUGUI)

“Kampeni hii inaweka malengo ya ukomo yanayotoa changamoto, lakini yanaweza kufikiwa. Sote tushirikiane kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2016, ni watoto, na sio wanajeshi.”