Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS/UNDP na WHO wasema tiba ya HIV iko mashakani

UNAIDS/UNDP na WHO wasema tiba ya HIV iko mashakani

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP na shirika la afya duniani WHO wanahofia mipango ya muda mrefu ya uwezekano wa kupatikana matibabu ya HIV ya gharama nafuu.

Katika taarifa ya sera iliyozinduliwa leo mashirika hayo yamezitaka nchi pale inapowezekana kutumia haki zao za sera za umiliki na uwezekano wa biashara zilizowekwa na mkataba wa shirika la kimataifa la biashara na azimio la Doha kuhusu afya ya jamii ili kupunguza gharama za madawa ya HIV na kupanua wigo wa watu wanaohitaji zaidi dawa hizo kuweza kuzipata.

Kwa mujibu wa UNAIDS wana wasiwasi na hatma ya mipango ya tiba ya HIV kwani ni theluthi moja tuu kati ya watu wanaohitaji dawa za kurefusha maisha ndio wanaozipata. Na limesema kwa mazingira ya sasa ya kiuchumi hata hao theluthi moja itakuwa vigumu kupata dawa hizo kwa muda mrefu.

Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2009 karibu watu milioni 15 walikadiriwa kuhitaji dawa za HIV za kurefusha maisha na watu milioni 5.2 pekee ndio wanaoweza kupata dawa hizo, huku mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea wakitegemea mgao wa bei nafuu wa dawa hizo.