Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njia bora za kilimo zinaweza kuongeza uzalishaji: De Schutter

Njia bora za kilimo zinaweza kuongeza uzalishaji: De Schutter

Wakulima wadogowadogo wanaweza kuongeza mara mbili uzalishaji wa chakula katika kipindi cha miaka 10 endapo watatumia mifumo ya ikolojia katika maeneo ambayo yanakabiliwa na njaa.

Hayo yameelezwa katika ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa ambayo inasema kilimo cha ikolojia hakitumii mbolea za viwandani lakini kinarutubisha udogo na kulinda mazao kutokana na wadudu waharibifu kwa kutumia mazingira asilia kama miti, mazao, wanyama na wadudu.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki ya chakula Olivier de Schutter amesema kwamba nchi ambazo sasa zinawekeza katika kilimo hususani Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara lazima zijikite katika kilimo cha ikolojia.

Amesema ujumbe wake ni kwamba matumizi ya mbolea na madawa ya viwandani vipunguzwe na watu waelimishwe kuhusu kilimo bora cha ikolojia kinachowafanya wakulima kutokuwa tegemezi na kuweza kuzalisha zaidi.