Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miezi sita baada ya mafuriko Pakistan hali bado ni mbaya:UNHCR

Miezi sita baada ya mafuriko Pakistan hali bado ni mbaya:UNHCR

Idadi kubwa ya wananchi wa Pakistan ambao walipigwa na mafuriko ya mwaka uliopita bado wanaendelea kuishi maisha ya taabu na dhiki kubwa ikiwa sasa imepita miezi sita tangu kutokea kwa mafuriko hayo mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo.

Inakadiriwa kwamba hadi sasa zaidi ya watu 166,000 bado wameendelea kukosa makazi na hivyo kufanya wasalie kwenye makambi 240 ambayo yametengwa kwenye maeneo mbalimbali. Mamia ya watu walipoteza maisha na mamia wengine kukosa makazi na kuharibiwa kwa miundo mbinu kufuatia mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo July 2010.

Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na mashirika ya kimataifa, lakini hata hivyo maaneo mengi bado hameendelea kusalia magumu kuishi na kukosa huduma muhimu za kijamii. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR hata hivyo limehaidi kuendelea kusalia nchini humo kwa ajili ya kutoa misaada zaidi katika maeneo ambayo huduma za kijamii bado ni mbaya.