Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa wito wa utulivu baada ya ghasia mpya Darfur

UM watoa wito wa utulivu baada ya ghasia mpya Darfur

Mkuu wa kikosi cha pamoja cha Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID Ibrahim Gambari ametoa wito wa kuwepo kwa utulivu baada ya makabiliano yaliyoshuhudiwa katika mji wa Nertiti ulio magharibi mwa jimbo la Darfur nchini Sudan.

Ghasia zilizuka siku ya Jumapili katika mji huo ulio umbali wa kilomita 63 mashariki mwa mji wa Zalingei baada ya afisa kutoka kitengo cha kitaifa cha ujasusi cha Sudan kuuawa na watu wasiojulikana. Kundi la UNAMID lililozuru eneo hilo baada ya ghasia hizo ili kupata habari kutoka kwa wenyeji lilibaini kuwa nyumba kadha zilikuwa zimeteketezwa huku maduka na masoko yakiwa yamefungwa .

Hata hivyo kwa sasa hali inatajwa kuwa tulivu na UNAMID inaendelea na shughuli za kila siku za kupiga doria. Hii leo baraza la usalama la Umoja wa Mataiafa limesema kuwa limesikitishwa kutokana na kuongezeka kwa ghasia na kuwepo ukosefu wa usalama katika jimbo la Darfur kikiwemo pia kisa cha kutekwa nyara kwa wafanyikazi watatu wa kitengo cha hewa cha kutoa huduma za kibinidamu tarehe 13 mwezi huu.