Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama limealaani mashambulio dhidi ya UNOCI

Baraza la usalama limealaani mashambulio dhidi ya UNOCI

Mashambulizi dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast UNOCI yamelaaniwa na wajumbe wa baraza la usalama.

Katika taarifa yao wameelezea hofu kuhusu kuendelea kwa machafuko na ukiukaji wa haki za binadamu katika taifa hilo la Afrika ya Magharibi. Rais wa baraza hilo balozi wa Bosnia na Herzegovina Ivan Barbalic amesema waliohusika na uhalifu huo dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia lazima wawajibishwe.

Amesema wajumbe wa baraza la usalama wanalaani vikali na kutaka kusitishwa mara moja matumizi ya vyombo vya habari kutoa taarifa potofu ili kuchochea chuki na ghasia , ikiwa ni pamoja na dhidi ya Umoja wa Mataifa. Wajumbe wanalaani mashambulizi dhidi ya walinda amani na raia.