Wataalamu wa haki za binadamu wa UM wahofia ukiukaji wa haki Ivory Coast

31 Disemba 2010

Wataalamu watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wanahofia sana kuendelea kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Ivory Coast wakati mvutano wa kisiasa ukiendelea.

Wataalamu hao wanasema duru za kuaminika zimethibitisha visa vya watu kutoweka, kuwekwa rumande, kutumia nguvu, mauaji na ubakaji vinafanyika na vinaweza kuendelea kutendeka nchini Ivory Coast.

Wameongeza kuwa vitendo hivyo vinapotendeka katika mazingira yanayosababisha watu kutoweka vinachukuliwa kama ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Wataalamu hao wameonya kwamba wote wanaohusika na ukatili huo lazima wawajibishwe.

Naye mwakilishi maalumu kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Rashida Manjoo amesema ukatili wa kimapenzi umekuwa ukitumiwa kama silaha za vita na wanawake na wasichana wamebaki bila ulinzi.

Ametoa wito kwa pande zote nchini humo kufanya kila liwezekanalo kuzuia ubakaji kuendelea, kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria na kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter