Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna sababu ya kujivunia katika vita dhidi ya ukimwi:Sidibe

Tuna sababu ya kujivunia katika vita dhidi ya ukimwi:Sidibe

Pamoja na kwamba vita vya ukimwi ndio vinashika kasi lakini mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe anasema kwa mara ya kwanza katika miongo mitatu maambukizi mapya ya HIV na vifo vimepungua kwa asilimia 20 duniani kote.

Nchi 56 ama zimeweza kudhibiti au kupinguza maambukizi mapya kwa kiasi kikubwa. Na kwa hatua hiyo Sidibe anasema kuna sababu ya kujivunia.

(SAUTI YA MICHEL SIDIBE)

Sidibe ameongeza kuwa mafanikio haya magumu yana hatihati na jukumu kupambana na ukimwi lazima lisalie katika hali ya juu.Hadi sasa watu wanaoishi na virusi vya HIV duniani ni milioni 33.3.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku hii amesema juhudi za jumuiya ya kimataifa za kuchukua hatua na kuokoa maisha ya watu zinaleta

mabadiliko duniani kote, anasema watu wachache ndio wanaombukizwa virusi na mamilioni ya watu wanapata fursa ya huduma na matibabu ya HIV.

Wanawake wengi wanaweza kuzuia watoto wao kupata virusi, vikwazo vya usafiri kwa wanaoishi na HIV vinaondolewa na nchi nyingi, unyanyapaa unaondoka japo taratibu na kutambuliwa kwa haki za binadamu. Ban amesisitiza pia haja ya kufikia malengo ya sufuri tatu, yaani maambukizi sufuri, ubaguzi sufuri, na vifo sufuri vitokanavyo na ukimwi.