Mabadiliko kwenye kilimo lazima kupunguza gesi chafu:Cancun

29 Novemba 2010

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala ya haki ya kupata chakula ameonya kuwa bila kuwepo kwa hatua madhubuti viwango vya gesi inayochafua mazingira vinavyotokana na kilimo vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia hamsini ifikapo mwaka 2030.

Olivier De Schutter amewasihi wanaohudhuria mkutano wa hali ya hewa mjini Cancun nchini Mexico kujadili masuala yanayombatana na sera za kilimo ili kupata suluhu kwa mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake kwa haki ya kupata chakula. De Schutter anasema majadiliano hayo yanayong'oa nanga hii leo yana umuhimu mkubwa ya kuwahakikishia mamilioni ya watu haki ya kupata chakula.

Inakadiriwa kuwa mazao yanayotokana na kilimo kinachotegema mvua kwenye nchi za kusini mwa afrika yanatarajiwa kupungua kwa asilimia hamsini kati ya mwaka 2000 na 2020 wakati ukubwa wa ardhi ya jangwa ikiongezeka kwa kati ya ekari milioni 60 na 90 kabla ya mwaka 2080. Wakati huo watu milioni 600 zaidi watakuwa bila chakula hali inayosababishwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud