Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umekaribisha mipango ya Congo kuanzisha sheria ya kwanza Afrika kulinda watu wa asili:

UM umekaribisha mipango ya Congo kuanzisha sheria ya kwanza Afrika kulinda watu wa asili:

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Congo kwa hatua kubwa inazochukua kutambua na kulinda haki za watu wa asili.

James Anaya ambaye amehitimisha ziara yake nchini humo hivi karibuni, amesema anatambua bado kuna changamoto kubwa, lakini kupiga hatua na kutekeleza mipango ambayo itasaidia kuboresha hali na maisha ya watu wa asili ni hatua kubwa.

Katika siku 11 za ziara yake nchini Congo bwana Anaya amesema amezuru jamii mbalimbali za watu wa asili katikia maeneo ya Likouala and Lekoumou, na kukutana na viongozi wa serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya jumuiya za kijamii mjini Brazzaville. Ameshukuru msaada wa serikali ya Congo hasa wizara ya sheria na haki za binadamu timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo kwa mipango ya kusaidia kufanikisha ziara hiyo.

Amesema amefurahishwa na mipango iliyokwisha wekwa na serikali kutekeleza haki za watu wa asili hasa ule wa kupitisha mswada ambao unatarajiwa kufanywa sheria kwenye mjadala wa bunge unaoendelea . Ikiwa sheria amesema itakuwa ya kwanza kabisa barani Afrika na inatoa mfano mzuri katika kanda hiyo kwa kutambua na kulinda haki za watu wa asili.