Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika kuadhimisha miaka 65 UM waahidi juhudi za kuleta amani na maendeleo

Katika kuadhimisha miaka 65 UM waahidi juhudi za kuleta amani na maendeleo

Jumapili Oktoba 24 Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa taarehe kama hiyo mwaka 1945.

Umoja huo umesema utajitahidi kuongeza juhudi za kuleta amani, maendeleo haki za binadamu na hatua za kutekeleza miapngo yake ya kimataifa. Tarehe 24 Oktoba ilitangazwa rasmi kuwa ni siku ya Umoja wa Mataifa kwani tarehe kama hiyo mwaka 1945 ndio siku ambayo mkataba wa Umoja wa Mataifa ulianza kutekelezwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akitoa ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku hiyo amesema siku ya Umoja wa Mataifa ni hafla ya kukumbusha maadili ya kimataifa ya kuvumiliana, kuheshimiana na kuheshimu utu wa mtu, pia kutathimini hatua zilizopigwa kwa pamoja katika masuala ya kufuta ujinga, umri wa watu kuishi, kusambaa kwa teknolojia, kukua kwa demokrasia na utawala wa sheria.

Ban ametoa wito wa kujitahidi zaidi kutekeleza mtazamo wa mkataba wa umoja wa Mataifa.

Ban ameongeza kuwa zaidi ya yote siku ya Umoja wa Mataifa ni siku ambayo tunaahidi kuongeza juhudi, ili kuwalinda waliokwama kwenye vita, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzuia zahma ya nyuklia. Pia kuongeza juhudi kutoa wigo mpana wa fursa kwa wanawake na wasichana na kukabiliana na mfumo isiyofuata haki na kukwepa mkono wa sheria.

Ban pia ametoa wito wa jitihada za pamoja ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya milenia yanafikiwa hasa kupunguza umasikini ifikapo mwaka 2015.