UM wataka nchi zilizoendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa nchi masikini

UM wataka nchi zilizoendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa nchi masikini

Umoja wa Mataifa umetaka mataifa yaliyoendelea kwa viwanda kuanza kutekeleza kwa vitendo ahadi zao za kuzipatia nchi zinazoendelea mabilioni ya dola ili ziweze kuchukua hatua juu ya mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza kwenye mkutano unaowakutanisha wataalamu mbalimbali wa kiafrika ikiwemo pia mawaziri huko Addis Ababa, Ethiopia, Katibu Mtendaji wa Kamishana ya uchumi kwa ajili ya bara la afrika ECA, Abdoulie Janneh amesema kuwa mataifa yaliyoendelea yanawajibika kutimiza ahadi hiyo sasa.

Amesema ahadi iliyotolewa na nchi hizo ya kwamba zitatoa kiasi cha dola bilioni 30 kuanzia mwaka 2010 hadi ifikapo 2012, ili kufikia shabaya ya kukusanya kiasi cha dola bilioni 100 ifikapo mwaka 2020,haina budi kuanza kutekelezwa sasa kwani itatoa ishara ya dhati namna nchi hizo zilivyomaanisha kutekeleza malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Suala la mabadiliko ya tabia nchi ni agenda muhimu katika majukwaa ya kimataifa hasa kwa kuzingatia namna dunia inavyopaswa kutenda kazi kwa pamoja ili kuzikabili changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi. Mkutano uliopita wa mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika Copenhagen ulifikia maazimio kadhaa ikiwemo hili la nchi zilizoendelea kiviwanda kutoa fedha zaidi kwa nchi maskini.