Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa zamani wa Chile ateuliwa kuongoza kitengo cha UM cha kuwawezesha wanawake UN-Women

Rais wa zamani wa Chile ateuliwa kuongoza kitengo cha UM cha kuwawezesha wanawake UN-Women

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amemteua na kumtangaza atakeyeongoza kitengo kipya cha wanawake cha Umoja wa Mataifa yaani UN-Women, ambaye ni Rais wa zamani wa Chile bi Michele Bachelet.

Bi Bachelet ataongoza kitengo hicho ambacho kwa sasa kitajumuisha ofisi na mashirika mengine manne ya Umoja wa Mataifa ambayo ni shirika la Umoja wa Mataifa la mfuko wa maendeleo kwa wanawake UNIFEM, kitengo cha maendeleo ya wanawake DAW, ofisi ya mshauri maalumu wa masuala ya jinsia na kitengo cha Umoja wa Mataifa cha utafiti wa kimataifa na taasisi ya mafunzo kwa maendeleo ya wanawake UN-INSTRAW.

Akimtangaza Bi Bachelet kushika jukumu la kuongoza UN-women Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema,

(SAUTI YA  BAN KI-MOON)

Ban ameongeza kuwa wiki ijayo kutakuwa na mkutano maalumu wa malengo ya maendeleo ya milenia na wanawake na watoto itakuwa ni ajenda kubwa katika kutoa msukumo wa kuhakikisha malengo ya maendeleo ya milenia yanafikiwa ifikapo mwaka 2015.

Kitengo hicho cha wanawake cha Umoja wa Mataifa ambacho kitakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na kilianzishwa rasmi tarehe pili Julai mwaka huu baada ya kupigiwa kura ya bila kupingwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa.