Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi wa Kenya kuongoza ofisi ya UM kwenye AU

Balozi wa Kenya kuongoza ofisi ya UM kwenye AU

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemteuwa balozi wa Kenya kuwa mkuu wa kwanza wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kwenye muungano wa Afrika AU.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Matifa ilianziwa mapema mwaka huu ili kuimarisha uhusiano baina ya Umoja wa Mataifa na AU. Zachary Muburi Muita ambaye alikuwa balozi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa hapa New York tangu mwaka 2006 amefanya kazi za kidiplomasia, kisiasa, kijamii , kijeshi na kushika nyadhifa mbalimbali kwa nchi yake tangu mwaka 1982.

Jukumu lake kubwa litakuwa kuimarisha uhusiano wa Umoja wa Mataifa na AU na pia mashirika ya kikanda. Wasifu wa Muburi- Muita unajumuisha pia kujihusisha na masuala mbalimbali kwenye jumuiya ya Afrika ya Mashariki , soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika COMESA na muungano wa serikali kwa ajili ya maendeleo IGAD. Ofisi mpya ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya AU ilianzishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa Julai mosi na makao yake makuu yatakuwa Addis Ababa Ethiopia yaliko makao makuu ya AU.