Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza kuu la UM limesikia wito wa kimataifa wa kuisaidia Pakistan iliyokumbwa na mafuriko

Baraza kuu la UM limesikia wito wa kimataifa wa kuisaidia Pakistan iliyokumbwa na mafuriko

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limekutana jioni hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kusikia kuhusu ukubwa , athari na mahitaji ya msaada kwa waathirika wa mafuriko nchini Pakistan.

Akizungumza kwenye mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema matatizo yanayoikabili Pakistan hivi sasa ni matatizo ya kimataifa na lazima kuwe na mshikamano kuwasaidia mamilioni ya wanaohitaji msaada.

Ban ameongeza kuwa takriban watu milioni 15 hadi 20 wanahitaji malazi, chakula, na huduma za dharura. Ikiwa ni wengi kuliko ukijumuisha pamoja waliokumbwa na Tsunami katika baharui ya Hindi,tetemeko la ardhi la Kashmir, kimbunga Nargis na tetemeko la karibuni la Haiti.

(SAUTI YA BAN PAKISTAN)

Ameongeza kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa , mashirika ya kiamatifa yasiyo ya kiserikali na makundi ya misaada kama shirikisho la msalaba mwekundu na mwezi mwekundu yamejitahidi kukusanya msaada kuisaidia serikali ya Pakistan. Naye waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Hillary Rodham Clinton amesema serikali ya Rais Obama na Marekani kwa ujuma wako tayari kuisaidia Pakistan na watu wake katika kipindi hiki kigumu kwa kila hali.

Mabalozi wa serikali mbalimbali kwenye Umoja wa Mataifa pia wameelezea nia na wito wa serikali zao kwa kushirikiana pamoja kunusuru maisha ya mamilioni ya watu walioathirika na mafuriko ambayo hajawahi kushuhudiwa kwa takribani miaka 80.