Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imewataka vijana kote duniani kujiunga na vita dhidi ya njaa

WFP imewataka vijana kote duniani kujiunga na vita dhidi ya njaa

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya vijana imewatolea wito vijana kote duniani kujiunga na mapambano dhidi ya njaa.

WFP inasema imetoa wito huo leo kwa kutambua umuhimu wa kizazi kijacho kutatua matatizo ya leo. Kuzinduliwa rasmi leo kwa mwaka wa kimataifa wa vijana kunaenda sambamba na kuanza kwa miradi ya miezi 12 ya WFP ya kuwawezesha vijana kote duniani ili wawe chachu ya mabadiliko.

Kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kote duniani WFP inawatia shime vijana kuvuka mipaka ya dini, siasa na tamaduni katika juhudi za kukabiliana na changamoto zinazowakumba binadamu kama njaa na umasikini. Mkurugenzi mkuu wa WFP Josette Sheeran amesema vijana ni muhimu sana katika vita dhidi ya njaa na viajana hawa ndio watakaomaliza tatizo la njaa duniani.