Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yakaribisha kuregezwa vikwazo dhidi ya wakimbizi wa Eritrea

UNHCR yakaribisha kuregezwa vikwazo dhidi ya wakimbizi wa Eritrea

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limekaribisha hatua ya kuregeza vikwazo kwa wakimbizi wa Eritrea walioko nchini Ethiopia.

UNHCR imesema imetowa moyo na uamuzi huo wa wiki jana wa serikali ya Ethiopia kuanzisha kile ilichokiita mradi wa nje ya kambi. Mradi huo utawaruhusu wakimbizi wa Eritrea kuishi nje ya kambi na katika sehemu yoyote ya nchi hiyo endapo wataweza kujikimu kifedha au wana jamaa au marafiki nchini Ethiopia wanaoweza kuwasaidia. Afisa wa UNHCR Andrej Mahecic amesema mabadiliko haya ya sera ni matokeo ya majadiliano ya shirika hilo na serikali ya Ethiopia yaliyolenga kuwawezesha wakimbizi wa Eritrea kuishi mazingira ya nje ya kambi.

Amesema tangu kuzuka kwa mfarakano wa mpaka baina ya nchi hizo mbili katika mwisho wa miaka ya 1990 zaidi ya wakimbizi wa Eritrea 60,000 wamevuka mpaka na kuingia Ethiopia. UNHCR inasema mbali ya kuwaruhusu wakimbizi hao kuishi katika mazingira ya mijini sera hiyo mpya itaimarisha pia uwezo wa wakimbizi wa eritrea kupata huduma muhimu na kujenga uhusiano na wenjeji.