Ban amelaani shambulio dhidi ya kituo cha michezo cha UNRWA Gaza

28 Juni 2010

Watu mbalimbali wamekuwa wakitoa kauli kufuatia shambulio la leo asubuhi Gaza dhidi ya kituo cha michezo ya kiangazi cha UNRWA.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani uvamizi huo na uharibifu na kusema anatiwa hofu kwani hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja tukio kama hilo linatokea. Katika taarifa yake iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu amesema mashambulio kama hayo ni kushambulia haki za watoto wa Gaza ambapo watoto 250,000 wanahudhuria michezo ya kiangazi ya UNRWA kwa ajili ya kujifunza na kupumzika kutokana na magumu ya kila siku kwenye ukanda wa Gaza.

Ban ameutaka uongozi wa Gaza kuzuia mashambulio yoyote dhidi ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kuhakikisha usalama wake , wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na programu za Umoja huo zinazowasaidia watu wa Gaza. Ametaka wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter