Skip to main content

Siku ya kimataifa ya kuwaunga mkono waathirika wa utesani Juni 26

Siku ya kimataifa ya kuwaunga mkono waathirika wa utesani Juni 26

Kesho Juni 26 ni siku ya kimataifa ya kuwaunga mkono waathirika wa utesaji na mataifa yote yana sheria ambazo zinapinga utesaji na kuufanya kuwa ni kosa.

Katika ujumbe wake kuhusu siku hiyo kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema pamoja na kwamba sheria zipo bado nchi nyingi utesaji unaendelea na wanaohusika hawachukuliwi hatua. Ameongeza nchi zinazofanya hivyo hujaribu kuuziba uhalifu huo ili usijulikane na kuwafanya wengi wafikirie kuwa haupo na hauwezi kutokea katika karne hii ya 21.

Jumatano wiki hii Pakistan imekuwa nchi ya 147 kuridhia mkataba wa kupinga utesaji na mifumo mingine ya kikatili , na sasa zimesalia nchi 45 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo hazijatia saini mkataba huo. Piallay amesema utesaji ni kosa kuwa chini ya sheria za kimataifa iwe ni katika wakati wa vita au wa amani.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika kuadhimisha siku hii ametoa wito kwa mataifa yote na watu wote kufanya kila liwezekenalo kukomesha mfumo wa utesaji ambao unashuha hadhi ya mtu, ni wa kikatili na ni ukiukaji wa haki na sheria.