Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za matumaini Gaza na Ukingo wa Magharibi muhimu kwa amani

Hatua za matumaini Gaza na Ukingo wa Magharibi muhimu kwa amani

Wakati mazungumzo ya awali yameanza baina ya Israel na Palestina, ni muhimu kuchukua hatua ambazo zitajenga kujiamini kwa Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

Tamko hilo la tahadhari limetolewa na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Robert Serry. Serry ameliambia baraza la usalama hii leo kwamba pande zote yaani viongozi wa Israeli na Palestina ameonyesha matumaini ya kisiasa kwa kuanza majadiliano hayo. Lakini ameonya kwamba matumaini haya sasa yatajaribiwa katika meza ya mazungumzo kabla ya kuwa na uwezekano wa mazungumzo ya ana kwa ana mapema iwezekanavyo.

Wakati huohuo Serry amesema Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na mamlaka ya Palestina, inatafuta mipango muafaka na mikubwa ya kuingilia ili kushughulikia mahitaji ya watu wa Gaza. Amesema kwanza maji na vyoo ni vitu ambavyo haviwezi kusubiri. Pili amesema UNRWA shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia Wapalestina linahitaji kujenga shule 100 Gaza kwa kuanza na 15 mara moja.