Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia iko mbioni kufikia malengo ya milenia ya maji safi ya kunywa

Dunia iko mbioni kufikia malengo ya milenia ya maji safi ya kunywa

Shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wamesema hivi sasa asilimia 87 ya watu wote duniani ambayo ni karibu watu bilioni 5.9 wanatumia maji safi ya kunywa.

Wamesema dunia iko mbioni au hata imepita malengo ya milenia ya watu kupata maji safi ya kunywa . Hii ni kutokana ripoti mpya ya mpango wa ushirikiano wa WHO na UNICEF waliyoiita "Ripoti ya maendeleo katika usafi na maji safi ya kunywa 2010" iliyotolewa leo.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema bado asilimia 39 ya watu wote duniani ambayo ni sawa na watu bilioni 2.6 wanaishi bila vifaa maalumu vya usafi kama vyoo, hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia malengo ya usafi ya milenia 2015.