Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yasema Umoja wa Mataifa hauna mpango wa kuitelekeza Somalia

OCHA yasema Umoja wa Mataifa hauna mpango wa kuitelekeza Somalia

Umoja wa mataifa hauna mpango wa kuitelekeza Somalia licha ya mazingira magumu yanayoambatana na vitisho na ghasia wanayokabiliana nayo wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.

OCHA ambayo ni Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura, imesema mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa bado yanaendesha shughuli zake kusini mwa Somalia licha ya kujiengua kwa WFP. WFP ambalo ni shirika la mpango wa chakula duniani limesema, shughuli za misaada ya kibinadamu bado zimesitishwa kusini mwa Somalia lakini shirika hilo limedhamiria kurejesha shughuli zake endapo watahakikishiwa usalama wa wafanyakazi wake.Akifafanua kuhusu usitishaji wa shughuli zao msemaji wa WFP Emilia Cassella amesema utendaji kazi yao umekuwa mgumu mno,.

" Ili kufafanua na kuhakikisha kila mtu anaelewa, WFP imesitisha operesheni zake Kusini mwa Somalia kwa muda, na hatua hii itawaathiri takribani watu milioni moja, lakini operesheni zetu zinaendelea katika maeneo mengine ya Somalia, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Moghadishu ambao ni makao ya watu wapatao milioni mbili. Hatujaondoka kabisa Somalia. WFP imekuwepo Somalia kwa karibu miaka 40 sasa, kwa hivyo hatuna mpango wa kuondoka Somalia.