Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MONUC akumbusha, vikosi vya UM katika JKK huhami maelfu ya raia kila siku

Mkuu wa MONUC akumbusha, vikosi vya UM katika JKK huhami maelfu ya raia kila siku

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), na pia Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) kwenye makala aliochapisha mapema wiki hii, katika gazeti la kila siku la Marekani linaloitwa The Washington Times, alieleza kwamba UM huchangisha pakubwa katika kuwatekelezea haki za kimsingi, takriban kila siku, kwa maelfu ya raia wanaoishi kwenye mazingira ya wasiwasi ya JKK.

Alisema kwa sababu ya kuwepo kwa vikosi vya UM kwenye maeneo husika, haki kimsingi za raia hufanikiwa kutunzwa na kulindwa. Taarifa ya Doss ilikusudiwa kujibu tetesi za kundi linalotetea haki za binadamu la Human Rights Watch, zilizodai vikosi vya UM katika JKK, vilishirikiana na wanajeshi wa taifa wa FARDC, ambao baadhi ya askari wao walituhumiwa "kutenda ukatili uliokiuka mipaka, dhidi ya raia" wakati walipokuwa wakiendeleza operesheni za kuwasaka waasi waliojificha kwenye maeneo kadha ya nchi. Wiki iliopita, Baraza la Usalama lilitoa mwito maalumu uliotilia mkazo umuhimu wa majeshi ya MONUC, kutumia "uwezo wote walionao" kuhakikisha raia wanaohatarishwa maisha na makundi ya aina yoyote yaliopo katika JKK, huwa wanapata hifadhi na ulinzi bora. Makala ya Doss ilisema vikosi vya MONUC vilipatiwa idhini ya Baraza la Usalama kusaidia kilojistiki jeshi la taifa la FARDC, katika operesheni za kushambulia waasi na kuwang'oa kutoka yale maeneo waliokuwa wamejificha na kutisha raia, operesheni ambazo zilihakikisha waasi hawatorejea tena kwenye sehemu hizi za nchi.