Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dunia wahimizwa na KM kuhudhuria Mkutano wa Copenhagen ili kuwasilisha mapatano ya kuridhisha

Viongozi wa dunia wahimizwa na KM kuhudhuria Mkutano wa Copenhagen ili kuwasilisha mapatano ya kuridhisha

Mapema Alkhamisi Msemaji wa KM alitoa taarifa maalumu kwa waandishi habari, kuhusu Mkutano Mkuu ujao wa UM juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, utakaofanyika mjini Copenhagen.

Kwenye taarifa hiyo, KM Ban Ki-moon alinakiliwa akikaribisha, kwa dhati, mwaliko wa Waziri Mkuu wa Denmark, Lars Lokke Rasmussen aliowatumia Viongozi wa Taifa na Serikali Wanachama uliowasihi wahudhurie Mkutano wa Copenhagen, angalau, katika siku za kufunga majadiliano. Kwa upande wake, KM naye pia alitangaza kauli yenye nguvu, yenye kuelezea natija zitakazopatikana pindi Viongozi wa Taifa na Serikali za Nchi Wanachama wa UM watajiunga kwenye mkusanyiko wa Mkutano wa Copenhagen kuanzia tarehe 17 mpaka 18 Disemba 2009. Alisema anaamini uhusiano wao, wa moja kwa moja, na wajumbe wa kimataifa watakaohudhuria mkutano utasaidia pakubwa serikali wanachama kufikia mapatano yanayofungamana na mizizi halisi, kwenye yale masuala yanayohusu taratibu zinazohitajika kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika ulimwengu.