Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Treni ya 'Climate Express' inaelekea Copenhagen kumurika umuhimu wa kuhitimisha mapatano ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa

Treni ya 'Climate Express' inaelekea Copenhagen kumurika umuhimu wa kuhitimisha mapatano ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa

Wanaharakati 400 ziada juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, wakijumlisha wapatanishi, viongozi wa mashirika ya kibiashara pamoja na watetezi wa hifadhi ya mazingira wanatarajiwa kusafiri pamoja kwenda Copenhagen kwa treni yenye jina la ‘Treni ya Hali ya Hewa ya Haraka\' (Climate Express), kwa madhumuni ya kuwahimiza viongozi wa dunia kufikia makubaliano yalio ya haki, yenye masharti ya kisheria na nia ya kutekelezwa, pale watakapokusanyika Denmark kuhudhuria mkutano mkuu wa UM juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Treni itaanzia mji wa Brussels, Ubelgiji, ikiwa ni hatua ya mwisho ya kutekeleza mradi unaojulikana kama ‘Mpango wa Treni ya Copenhagen'. Mradi huu ulilitayarishwa na Chama cha Wafanyakazi wa Kimataifa wa Reli (UIC), wakiungwa mkono na ile kampeni ya UM ya ‘Kufunga Makubaliano ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa' pamoja na Tassisi ya Mfuko wa Kuhifadhi Maliasili Duniani (WWF), ambalo hushughulikia hifadhi ya jumla ya mazingira.