Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumaa asubuhi KM Ban Ki-moon, akijumuika na wafanyakazi wa UM waliopo kwenye Mkao Makuu, pamoja na maofisa wa vyeo vya juu, ikijumlisha Naibu KMAsha-Rose Migiro walikusanyika kwenye Ukumbi wa Baraza la Udhamini kuwakumbuka watumishi wenziwao watano waliouawa Ijumatano, na wapinzani wa Taliban, ndani ya nyumba ya wageni, kwenye mji wa Kabul, Afghanistan. Watumishi waliouawa walitokea Philippines, Marekani, Ghana na Liberia. Mtu wa tano hajatambuliwa bado uraia wake, ikisubiriwa matokeo ya vipimo vya afya vinavyoendelezwa na madakatari kuthibitisha asili ya maiti. Kabla ya wafanyakazi wa UM kusikiliza taarifa ya KM juu ya tukio, na miradi inayoandaliwa kuimarisha usalama wa watumishi wa UM waliopo nje, hasa katika Afghanistan, walisimama wima kimya kwa dakika moja kuwakumbuka na kuwaombea wenziwao waliouawa na shambulio la bomu la kujitoa mhanga. Baadaye mke wa askari wa usalama aliyeuawa kutoka Ghana alihutubia mkusanyiko huo na aliomboleza juu ya kifo cha mumewe, marehemu Lawrence Mefful. Kwenye risala yake, KM alisema UM sasa hivi unafanya mapitio ya dharura juu ya mazingira ya usalama, kwa ujumla, nchini Afghanistan. Alisema UM unazingatia vile vile uwezekano wa kupeleka vikosi ziada vya usalama kuhakikisha majengo ya UM yanapatiwa ulinzi na hifadhi bora kujikinga na mashambulio.

Ofisi ya KM imetangaza leo kwamba wataalamu watatu wameteuliwa na KM kuwakilisha Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi kwa Guinea, yenye lengo la kutafuta ushahidi hakika wa matukio ya tarehe 28 Septemba 2009 katika mji wa Conakry, Jamhuri ya Guinea ambapo iliripotiwa raia 150 ziada waliuawa. Tume itajumlisha Mohamed Bedjaoui wa Algeria, atakayeongoza shughuli za bodi la uchunguzi, pamoja na Françoise Ngendahyo Kayiramirwa wa Burundi, na vile vile Pramila Patten wa Mauritius. Bedjaoui ni mwanadiplomasiya na mwanasheria mashuhuri; Kayiramirwa ni Waziri mstaafu wa Ushikamano wa Taifa, Haki za Binadamu na Jinsiya na Bi. Patten ni mwanachama wa Kamati ya UM ya Kufyeka Ubaguzi wa Rangi Duniani. Wajumbe hawa watatu wa Tume ya Kimataifa ya Uchunguzi kwa Guinea wanatazamiwa kuelekea New York katika siku za karibuni kukutana na KM, na baada ya hapo watakwenda Geneva na halafu Guinea kuendeleza shughuli zao, na watasaidiwa kwenye kazi zao na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu.

Michael Williams, Mratibu Maalumu wa UM kwa Masuala ya Lebanon , leo alionana na Ammar Moussawi, mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa wa Hizb'Allah. Baada ya mkutano alisema UM umeingiwa wasiwasi juu ya matukio ya karibuni katika Lebanon kusini, ikijumlisha tukio la madai ya kurushwa makombora kutoka kijiji cha Houla, ikifuatiwa na majibu ya mashambulio ya majeshi ya Israel dhidi ya tukio hilo. Williams alikhofia vitendo hivyo vina uwezo wa kuzusha, kwa urahisi, hali ya mtafaruku na vurugu katika Lebanon kusini. Kadhalika, Ijumatano Williams alikutana kwa mazungumzo na Dktr. Samir Geagea na walisailia maendeleo katika bidii ya kubuni serikali mpya ya taifa, juhudi ambazo zimeshindwa kukamilishwa, miezi mitano kufuatia uchaguzi wa bunge wa tarehe 07 Juni 2009.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti tarehe ya leo, 30 Oktoba 2009, ni tarehe ya kihistoria baada ya kufanikiwa kuhitimisha operesheni za muda mrefu za kufarajia wahamiaji 400 wa mwisho wa Burundi, waliosalia kwenye makazi ya muda nchini Tanzania. Raia hawa wa Burundi walihajiri makwao kunusuru maisha na kujiepusha na fujo zilizozuka nchini katika mwaka 1972. Wahamaji walitarajiwa kuondokea kutoka makazi ya muda ya Katumba, yaliopo sehemu za magharibi katika Tanzania, opereshini iliokamilisha mradi wa mwaka na nusu wa kuwarudisha makwao, kwa khiyari, nchini Burundi. Kuanzia Machi 2008, UNHCR ilishirikiana na Serikali ya Tanzania kuwasaidia raia wahamiaji wa Burundi kurudi nchini mwao. Vile vile chini ya mpango huu, wahamiaji wa Burundi 162,000 walisajiliwa kuomba uraia wa Tanzania na inaripotiwa katika mwezi Agosti wahamiaji 29,000 waliandikishwa rasmi uraia. Serikali ya Tanzania sasa hivi inatazamia kukamilisha mpango wa kuandikisha uraia kwa wahamiaji wa Burundi waliosalia katika mwisho wa mwaka. Baada ya hali ya usalama na utulivu kurejea Burundi, ijapokuwa kwa kusota, wahamiaji raia zaidi ya nusu milioni waliokuwepo nje ya Burundi, walirudi makwao, ikijumlisha wahamiaji 430,000 kutoka kambi za makazi ya muda katika Tanzania.