Hapa na pale

Hapa na pale

KM amemteua Dktr. David Nabarro kuwa Mjumbe M aalumu juu ya Udhibitaji Bora wa Lishe na Chakula duniani. Jukumu la Dktr. Nabarro hasa litakuwa ni kumsaidia KM kuhimiza mataifa kutumia miradi ya kizalendo ya kujitegemea chakula maridhawa na udhibiti bora wa lishe, kwa kufuata taratibu za jumla, zenye malengo yalioratibiwa kujumuisha kipamoja mchango muhimu wa mashirika ya kimataifa, ili kukuza misaada inayohitajika kutekelza huduma hizo kwa mafanikio. Tangu mwezi Januari mwaka huu, Dktr. Nabarro alidhaminiwa madaraka ya kushughulikia masuala yanayohusu chakula, na kuandaa taratibu za kuimarisha akiba ya chakula duniani kwa madhumuni ya kutosheleza mahitaji ya umma wa kimataifa.

Asubuhi, Baraza la Usalama lilifungua rasmi shughuli zake, kwa kuitisha kikao cha faragha, ambapo wajumbe wa Baraza walisikiliza taarifa maalumu kutoka Raisi wa Mahakama ya Kimataifa (ICJ), Hisashi Owada juu ya kazi za taasisi hiyo. Baada ya hapo Baraza la Usalama lilipitisha azimio la kuongeza muda wa vikwazo vilivyoekewa Cote d'Ivoire, kwa mwaka mmoja zaidi. Kadhalika, Baraza la Usalama lilizingatia ripoti ya kila mwaka inayotumiwa Baraza Kuu la UM juu ya shughuli zake. Ijumatano, Baraza la Usalama lilipitisha Taarifa ya Tamko la Raisi (Presidential Statement) ya kuyakaribisha makubaliano ya Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) yaliounga mkono uamuzi wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon wa kuanzisha bodi la uchunguzi la kimataifa, kutathminia mauaji ya raia yaliotukia tarehe 28 Septemba 2009 katika Guinea. Kabla ya Baraza kuchukua uamuzi huo walitia maanani kwamba wenye mamlaka Guinea walishaahidi rasmi kuwa watalisaidia bodi la uchunguzi la kimataifa kutekeleza kazi zake kama inavyopasa na kuwapatia wajumbe wa tume hifadhi inayofaa. Baraza la Usalama, kwa upande wake, limelaani vikali fujo zilizozuka Guinea mwisho wa Septemba, hali ambayo inaripotiwa ilisababisha vifo vya raia 150 na mamia ya majeruhi, ikijumlisha pia na makosa karaha ya kujamii kimabavu wanawake, ikichanganyika na jinai ya ya kijinsia dhidi ya wanawake.

Henry Anyidoho, Kaimu Mkuu wa Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) aliripotiwa kuwa na mazungumzo mjini Khartoum na maofisa wa vyeo vya juu wa Serikali ya Sudan juu ya masuala kadha ya kikazi, ikijumlisha taratibu za kuchukuliwa kudhibiti ujambazi na vitendo vya uhalifu vinavyofanyika katika jimbo la Darfur. Wakati wa majadiliano na Ibrahim Mahmoud Hamid, Waziri wa Mambo ya Ndani na Al Saman Al Wasila, Waziri wa Nchi juu ya Masuala ya Nchi, Kaimu Mkuu wa UNAMID alijadilia nawo suala linalohusu watumishi wa UNAMID waliotekwa nyara na ambao hivi sasa wanaendelea kushikwa na makundi yasiotambuliwa katika Darfur, akijumuika pia mtumishi mmoja wa Kamati ya Msalaba Mwekundu (ICRC) aliyenyakuliwa huko katika siku za karibuni. Anyidoho aliiomba Serikali ya Sudan kuongeza bidii katika kuhakikisha mateka hawo wataachiwa haraka, na bila kujeruhiwa, na pia kuitaka Serikali kuchukua hatua za kidharura kukomesha matatizo ya kuteka nyara watu katika Darfur.

Ripoti mpya ya KM juu ya hali katika Guinea-Bissau na shughuli za Ofisi ya UM juu ya Usaidizi wa Kujenga Amani nchini, inayotolewa kila baada ya miezi mitatu, ilichapishwa Alkhamisi leo, ambamo KM aliupongeza umma wa Guinea-Bissau, Kamisheni ya Uchaguzi ya taifa pamoja na vikosi vya usalama na majeshi ya ulinzi, kwa mchango wao uliohakikisha uchaguzi wa taifa uliofanyika miezi ya Juni na Julai mwaka huu, uliendelezwa kwa utaratibu uliopangwa vizuri na usio na fujo, hasa baada ya kufuataia mauaji ya kisiasa ya viongozi muhimu yaliotukia mnamo mwanzo wa mwaka. Vile vile KM alisema kwenye ripoti ameingiwa matumaini juu ya kutengenea zaidi kwa hali, kwa ujumla, katika Guinea-Bissau baada ya Bunge la Taifa kuitisha mkutano maalumu kuzingatia suluhu ya vyanzo vya mizozo na hali ya kisiasa isiotulia katika Guinea-Bissau. KM pia alibainisha kuridhika kwake kwa uamuzi wa raisi mpya mteule wa Guinea-Bissau, Malam Bacai Sanha pamoja na Serikali kuahidi kuwa watafanyisha uchunguzi maalumu juu ya mauaji ya kisiasa yaliotukia mwanzo wa mwaka. Vile vile KM aliridhika na dhamira ya wenye madaraka kukomesha tabia ya kuendeleza mauaji ya kihorera nchini bila kukhofia adhabu, na kuhakikisha kunakuwepo haki na kupatikana upatanishi wa taifa.