Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban anasema kiwango cha uwambukizaji wa kifua kikuu kinapungulia

Ban anasema kiwango cha uwambukizaji wa kifua kikuu kinapungulia

Akiadhimisha siku ya kifua kikuu duniani hii leo, KM Ban Ki-moon amesema kasi za kupungua ugonjwa wa kifua kikuu zinakwenda pole pole na kuonya kua juhudi za kupambana na ugonjwa huo zinapunguka.

Ripoti mpya ya shirika la Afya Duniani WHO inaeleza kwamba, kiwango jumla cha watu wanaoambukizwa na ugonjwa huo wa hatari kimepunguka kutokea watu 142 kwa kila watu laki moja hapo 2004, na kufikia 137 kwa kila watu laki moja. Katika ujumbe wake Bw Ban amesema, ingawa kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana, na mamilioni ya watu wananufaika na matibabu kupitia utaratibu wa juhudi za kitaifa, lakini anasema mamilioni zaidi hawapati tiba. Alionya kwamba, bila ya kuchukuliwa hatua za haraka idadi ya wanaoambukizwa itaendelea kuongezeka kutokana na ugonjwa huo unaosababisha kifo cha mtu moja kila sekunde 20. Akitoa ripoti ya utafiti, mkurugenzi wa WHO, Margaret Chan amesema utafiti unadokeza haja ya kuchukuliwa hatua za dharura kutafuta, kuzuia na kutibu kifua kikuu miongoni mwa watu wanaoishi na virusi vya HIV na kuwapima wagonjwa wote ikiwa wana virusi vya HIV ili kuweza kutoa tiba na huduma. Bi Chan aliyahimiza mataifa kuimarisha ushirikiano kupambana na magonjwa hayo mawili, na ni lazima kuzuia watu wenye HIV kufariki kutokana na kifua kikuu.