Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana milioni 115 duniani ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika

Vijana milioni 115 duniani ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika

Miaka 50 tangu kuanza maadhimisho ya siku ya kujua kusoma na kuandika duniani, maendeleo yamefikiwa lakini bado kuna changamoto kwa kila mtu kujua kusoma na kuandika.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kisomo duniani  hii leo akisema kuwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 750 duniani kote ni wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika.

Kati yao hao milioni 115 ni vijana na hivyo kuwa ni kikwazo katika kufanikisha ajenda 2030 ambayo kwayo kujua kusoma na kuandika ndio kitovu chake.

Kwa mantiki hiyo amesema vikwazo hivyo kwa maendeleo endelevu vinaweza kuondolewa kwa kutunga sera sahihi zinazopatiwa kichochea na rasilimali za kutosha.

Mathalani amesema ni lazima kuhakikisha watoto ambao hawako shuleni wanapata fursa ya kujifunza, sambamba na kuboresha elimu inayotolewa na kuendeleza elimu ya watu wazima.