Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wazima na watoto wapunguze matumizi ya sukari: WHO

Watu wazima na watoto wapunguze matumizi ya sukari: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetoa mwongozo mpya kuhusu matumizi ya sukari miongoni mwa watoto na watu wazima kwa lengo la kuimarisha afya na kuepusha magonjwa. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

WHO inapendekeza matumizi ya sukari kwa siku yawe chini ya asilimia 10 ya kiwango chote cha mlo wa kutia nguvu mwilini na kama ikiwezekana punguzo la nyongeza la vijiko sita vya chai vya sukari.

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na lishe kwa afya na maendeleo Dokta Francesco Branca amesema kuna ushahidi thabiti kuwa mtu akizingatia kiwango hicho anaepukana na utipwatipwa na kuoza kwa meno.

Sukari husika ni zile zinazoongezwa kwenye vyakula na vinywaji, jikoni wakati wa mapishi au wakati wa kunywa chai na ile iliyoko kwenye asali na maji ya matunda kutoka viwandani.

WHO inapendekeza mabadiliko ya sera ili kuwezesha nchi kuzingatia azma yao ya kupunguza matumizi ya sukari ambayo yanaongeza mzigo wa magonjwa yasiyoambukizwa.

Hata hivyo WHO inasema mwongozo huo mpya wa matumizi ya sukari haugusi sukari iliyomo kwenye matunda, mboga na maziwa kwa sababu hakuna ushahidi kuwa matumizi yake yana madhara kwa walaji.