Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utamaduni wa kupinga machafuko unaanzia kwenye jamii:Ban

Utamaduni wa kupinga machafuko unaanzia kwenye jamii:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kazi ya kuunda na kudumisha amani na kupinga machafuko ni utamaduni unaoanzia katika mioyo ya watu binafsi wanawake na wanaume.

Ban ameyasema hayo katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga machafuko ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba pili.  Ban amesema amani huenda ikapatikana kwa njia ya mazungumzo, lakini inadumishwa na jamii inayoizunguka, ameongeza kuwa amani inaanzia kwa watu, kutoka katika mioyo ya wanawake na wanaume,jamii, familia na watu binafsi wote wana jukumu kubwa katika kuyashinda machafuko na kujenga utamaduni wa kukumbatia amani.

Amesema kazi hiyo haiwezi kuachwa kwa serikali ay mashirika ya kimataifa pekee. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unatumia kila njia kuhakikisha unayashinda machafuko hasa kwa kuchaguza masuala ya haki za binadamu, kutatua migogoro kwa njia ya amani, kufanya kampeni kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, kujitahidi kufikia malengo ya maendeleo ya milenia na kuwa kama daraja miongoni mwa tamaduni na dini mbalimbali ili kukabiliana na matatizo ya chuki na itikadi kali.

Siku hiyo pia inakwenda sabambamba na tarehe ya kuzaliwa Mahatma Gandhi kiongozi wa vuguvugu la uhuru wa India na kinara wa dhana na mikakati ya kupinga machafuko . Ban ametoa wito wa ushirikiano na kutumia nguvu ya kupinga machafuko kuchagiza amani kwa ajili ya jamii zetu na watoto wetu.

Siku ya kimataifa ya kupinga machafuko ilianzishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa kama siku ya kusambaza ujumbe wa kupinga machafuko kwa njia ya elimu na kuielimisha jamii na ilianza kuzdhimishwa rasmi mwaka 2007.