Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi za wakimbizi Tigray zasambaratishwa- UNHCR

Picha ya maktaba ya kambi ya wakimbizi ya Shemelba jimboni Tigray nchini Ethiopia
© UNHCR/Frederic Courbet
Picha ya maktaba ya kambi ya wakimbizi ya Shemelba jimboni Tigray nchini Ethiopia

Kambi za wakimbizi Tigray zasambaratishwa- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR hatimaye limeweza kuingia katika kambi za wakimbizi za Shimelba na Hitsats zilizoko jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethopia, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwezi Novemba mwaka jana wa 2020 mapigano yalipoanza.

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi Boris Cheshirkov amewaambia waandishi wa Habari kuwa katika ziara ya Pamoja ya watendaji wa shirika hilo na wale wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, walibaini kuwa kambi zote zimeharibiwa kabisa, na vifaa vyote vya misaada ya kibinadamu vimeporwa na vingine kuharibiwa.

Mathalani katika kambi ya Hitsats, ujumbe huo ulibaini kuwa makazi yote na nyuma vimeteketezwa kwa moto, huku picha za setilaiti na simulizi za wakimbizi zikidokeza hicho kilichotokea.

Hata hivyo hadi sasa hawajabaini nani amehusika na vitendo hivyo.

Ujumbe huo pia, kwa mujibu wa Cheshrkov ulitembelea mji wa Shiraro ambako wakimbizi wamesambaa huku na kule wakisaka msaada wa dharura na usaidizi.

Msemaji huyo ameongeza kuwa ujumbe mwingine utakwenda eneo hilo kubaini idadi ya watu wanaoishi eneo hilo kwa sasa na iwapo UNHCR na ofisi ya Ethiopia ya masuala ya wakimbizi na warejeao wanaweza kutoa msaada eneo hilo na mipango ya kuwahamishia maeneo mengine.

Bwana Cheshirkov amesema, “UNHCR ina wasiwasi mkubwa sana juu ya ustawi wa wakimbizi kutoka Eritrea ambao wawamekuwa wakiishi eneo hilo na ambao sasa wamekimbia kusaka usalama.”

Takribani wakimbizi 20,000 wamekuwa wakiishi kwenye kambi hizo mbili kabla ya janga kuanza mwezi Novemba mwaka jana, wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipoanzisha kampeni ya kijeshi dhidi ya eneo la Tigray akishutumu chama tawala jimboni humo, TPLF kushambulia kambi za kijeshi.

Kwa mujibu wa Cheshirkov zaidi ya wakazi wa zamani 7,000 wa kambi hizo mbili wamesaidiwa na mamlaka za Ethiopia au wao wenyewe kukimbilia kambi nyingine za Mai Aini na  Adi Harush.

Taarifa za hivi karibuni zaidi kuhusu kuharibiwa kwa kambi hizo zinakuja wakati maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa wakitoa wito wa kumalizika kwa mapigano, huku ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ikitaka uchunguzi wa madai ya ukiukwaji mkubwa wa hak iza binadamu unaofanywa na pande zote huko Tigray.

Hii leo Waziri Mkuu Abiy ametumia mtandao wa Twitter kusema kuwa serikali ya Eritrea imekubali kuondoa vikosi vyake kutoka Tigray na kwamba vikosi vya Ethiopia vitahusika na ulinzi wa maeneo ya mpakani kuanzia sasa.