UNHCR yaitaka Ethiopia kuruhusu kufikiwa wakimbizi 96,000 wasio na chakula Tigray

1 Disemba 2020

Shirika la Umoja wa Mastaifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limeiomba serikali ya Ethiopia kulipa ruhusa ya dharura ili kuweza kuwafikia wakimbizi 96,000 kutoka Eritrea waliokwama kwenye jimbo la Tigray ambao sasa hawana huduma muhimu ikiwemo chakula kutokana na machafuko yanayoendelea kwa mwezi mmoja sasa. 

Babar Baloch ambaye ni msemaji wa UNHCR mjini Geneva amesema “Wakati hofu yetu ikiongezeka kila saa tunaiomba serikali kuu ya Ethiopia watupe fursa ya haraka kuingia kwenye jimbo la Tigray ili kuwafikia watu wanaohitaji msaada haraka. Makambi kwa sasa yatakuwa yameishiwa chakula na kufanya njaa na utapiamlo kuwa hatari kubwa.” 

Msemaji huyo ameongeza kuwa “Pia tumeshtushwa na taarifa ambazo haijathibitishwa za mashambulizi, utekaji na kushinikiza watu kuingia katika mapigano kwenye makambi ya wakimbizi.” 

Bwa. Baloch hata hivyo amesema ni vigumu kuthibitisha hali ya sasa na UNHCR haijaweza kuwasilina na wakimbizi kutoka Eritrea tangu kuzuka kwa mzozo wa sasa Tigray mwamzoni mwa mwezi Novemba. 

Wakimbizi wamekuwepo muda mrefu 

Kwa mujibu wa UNHCR Ethiopia imekuwa ikihifadhi wakimbizi kutoka Eritrea katika makambi manne ya wakimbiz kwa zaidi ya muongo mmoja, lakini sasa kuna ripoti kwamba wakimbizi hao wa Eritrea wametawanywa ndani ya jimbo la Tigray. 

Jumatatu wiki hii kamishina mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi alizindua ombi la dola milioni 147 ili kukidhi mahitaji ya raia wa Ethiopia zaidi ya 43,000 ambao wamekimbia mapigano katika jimbo la Tigray na kuwa wakimbizi katika nchi jirani ya Sudan na idadi yao ikitarajiwa kuongezeka na kufikia 100,000 ifikapo mwezi Aprili mwakani. 

Hata hivyo Baloch amesema idadi ya raia hao waliomiminika Sudan imefika 46,000 lakini kwa sasa wimbi linaloingia linapungua huku wakimbizi wapya wakielezea kuwepo na vizuizi vya barabarani kati ya Ethiopia na Sudan na kufanya kuwa vigumu wao kupita.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter